top of page

Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Kibosho
ST. MARY'S PARISH KIBOSHO

 Kaeni ndani yangu nami ndani yenu (Yohane 15:4)

Historia ya Parokia yetu

HISTORIA FUPI YA PAROKIA YA B.MARIA MPALIZWA-KIBOSHO Unapoingia katika Kanisa zuri la Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni lililopo katika Parokia ya Kibosho unakutana na maneno haya matakatifu yaliyopo mbele ya Kanisa (chini ya mchoro mtakatifu wa Yesu Kristo aliyeshika kitabu cha Injili kwa mkono wake wa kushoto, na pia mkono wake wa kuume ukiwabariki wote waingiao Kanisani). Ndugu msomaji wa hisoria hii, ninapenda kutoa ufafanuzi mfupi wa maneno haya ili tuelewe kwa undani maadhimisho ya miaka 125 ya Ukristo katika eneo la Kibosho. Maneno haya matukufu yalitamkwa na Yesu Kristo mwenyewe, hivyo tunawajibika kuyashika kwa uaminifu na kuyatekeleza kwa upendo. Hapa Bwana wetu Yesu Kristo kwanza anajipa wajibu wake wa kukaa ndani ya wanafunzi wake, pili anawapatia wanaomwamini (matawi) wajibu wa kuungana na Mzabibu wao wa Kweli Yesu Kristo. Kimsingi huu ndio wito wa ubatizo wetu: kukaa na kuishi ndani ya Kristo. Tukumbuke kwamba kila mfuasi anatambulika katika kukesha katika Kristo na kuwa na ushirika naye. Wale wote wanaojiita Wakristo lazima maisha yao yajikite kwa Kristo. Nasi Wakibosho tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya miaka 125 ambayo Kristo amekaa ndani yetu, jumuiya zetu, familia zetu, tamaduni zetu, mila zetu na katika mioyo yetu. Halafu pia tunamrudishia Mungu shukrani kwa Baraka ya miaka 125 amabayo Wanakibosho wameishi ndani ya Kristo. Tumeishi na kukaa ndani ya Kristo kupitia Neno la Mungu ambalo limekuwa taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Rejea Zaburi 119:105). Pia tumekaa ndani ya Kristo kupitia Sakramenti zilizowekwa na Kristo ambazo zinaendelea kutakatifuza mioyo yetu ili kutuweka tayari kwa ajili ya kujiandaa kwa JUBILEI YA MILELE yaani FURAHA YA MILELE MBINGUNI. Katika miaka hii 125 tunaunganika na maneno ya Mt. Paulo kwa Wagalatia alipowaambia LAKINI MIMI, HASHA, NISIONE FAHARI JUU YA KITU CHOCHOTE ILA MSALABA WA BWANA WETU YESU KRISTO, AMBAO KWA HUO ULIMWENGU UMESULUBISHWA KWANGU, NAMI KWA ULIMWENGU (Wagalatia 6:14). Hivyo sisi Wakibosho fahari yetu ipo katika msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo uliosimikwa miaka 125 iliyopita na Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu. YESU KRISTO NI YEYE YULE, JANA NA LEO NA HATA MILELE JESUS CHRISTUS HERI ET HODIE IPSE ET IN SAECULA WAEBRANIA 13:8 1.1. WAMISIONARI WA ROHO MTAKATIFU WANAINGIA KIBOSHO Akiwa na lengo la kuanzisha kituo cha Wapolishi Wakatoliki, Bwana Herr Von Eltz (msimamizi wa kituo cha kijerumani Moshi), alizungumza na Mhashamu Askofu de Courmont, Askofu wa Vikarieti ya Zanzibar, ili amtume Padre kuhudumu maeneo ya Moshi. Maandalizi ya kuja Moshi yalianza mwaka 1888. Mwaka 1890 Askofu de Courmont na Mapadre Le Roy na Commenginger walifika maeneo ya Mlima Kilimanjaro. Shirika la Mapadre wa Roho Mtakatifu lilianzishwa huko Ufaransa mnamo 27 Mei 1703 likiwa chini ya ulinzi wa Moyo Safi wa Bikira Maria (Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili). Utume wa Shirika hili ulijikita nje ya Ufaransa (duniani kote hasa bara la Afrika ambapo Ukristo ulikuwa haujaota mizizi). Karama ya Shirika ilikuwa ni kuinjilisha kwa watu maskini na waliotengwa na jamii. Na pia kuinjilisha kule ambapo Kanisa lilipata mazingira magumu. Kwa ujasiri mkubwa walipokuja Afrika walikuwa na lengo la kuinjilisha kwa kuwafanya huru watumwa. Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu waliingia eneo la Afrika Mashariki wakitokea katika kisiwa cha Reunion ambako huko waliwakomboa watumwa wengi. Mapadre hawa walinuia kufika kwanza kabisa katika kisiwa cha Zanzibar, na mwaka 1860 walipewa ruhusa na uongozi wa Kanisa wa kufanya kisiwa hicho kuwa kituo kikuu cha utume wao. Hapo Zanzibar waliweka kambi yao karibu na soko la watumwa mwaka 1893, na mwaka 1868 walianzisha kituo kingine cha utume huko Bagamoyo. Bagamoyo ndio ikawa mlango wa imani kwa eneo lote la bara. 1.2.ASKOFU JEAN MARIE RAOUL DE COURMONT WA VIKARIETI YA ZANZIBAR ANAFIKA KILIMANJARO Uamuzi wa kufanya ziara Kilimanjaro ulichukuliwa na Askofu Jean Marie Raoul de Courmont wa Vikarieti ya Zanzibar. Kwa nyakati hizo, Vikarieti ya Zanzibar ilifika mpaka Dodoma, Mbulu, Kilimanjaro, Tanga, Mombasa hadi Nairobi. Kwa ujio wake Kilimanjaro, Askofu de Courmont alikuwa akifanya ziara ya kitume katika Vikarieti yake. Julai 1890 Askofu huyu alianza maandalizi ya safari ya kimisionari kuelekea Kilimanjaro. Lengo lake kuu ilikuwa ni kuleta mwanga wa Injili kwa mara ya kwanza Kilimanjaro, na pia kutafuta sehemu nyingine za kufikisha Injili nje ya Kilimanjaro. Aliwachagua Mapadre wawili wa kusafiri nao: Padre Auguste Commenginger na Padre Alexander Le Roy, waliandamana na wabeba mizigo, wapishi, wakalimani na watu ambao waliowaongoza njia. Walisafiri toka Zanzibar hadi Mombasa ambapo walifika tarehe 10 Julai 1890. Hapo Mombasa hawakujua ni njia ipi inayoelekea Kilimanjaro. Lakini kwa bahati njema, huko Mombasa kulikuwa na kijana mmoja aliyefanya shughuli za kibiashara (biashara ya kubadilishana pembe za ndovu na bidhaa za kifahari zilizopatikana pwani ya Mombasa), huyu nyumbani kwake kiasili kulikuwa Kilimanjaro eneo la Kilema. Jina lake aliitwa NDERINGO. Alisafiri na Wamisionari hao tarehe 15 Julai 1890 wakipitia sehemu iitwayo Likoni. Kutoka hapo walipita sehemu za Digo, Vanga, Gasi, Mafisi,, Mwadunda, Kikome, Duluni, Mbarara, Kilumbi, Kitivo, Usambara, Gonja, Kisiwani, Usangi, Ugweno, kandokando mwa Ziwa Jipe. Walipofika Ziwa Jipe waliuona Mlima Kilimanjaro. Tarehe 14 Agosti 1890 msafara wa Wamisionari ulikuwa bado maeneo ya Taveta. Ilikuwa hamu ya Askofu Courmont kufika katika miteremko ya Mlima Kilimanjaro tarehe 15 Agosti, ili aadhimishe Misa kwa heshima ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni katika ardhi ya Wachagga. Kwa tendo hilo aliukabidhi Mlima Kilimanjaro chini ya ulinzi wa Bikira Maria. Hiyo Misa waliisali chini ya vivuli vya miti miwili mikubwa kandokando ya mto. Tarehe 16 Agosti walivuka mto mkubwa wa Himo (Ghona), Nderingo akawapeleka moja kwa moja kwa Mangi Fumba. Wamisionari walipokewa vizuri sana huko Kilema, kisha wakaweka kituo cha uinjilishaji huko Kilema. 1.3.KILEMA HADI MACHAME Toka hapo Kilema, Wamisionari hawa watatu tarehe 18 Agosti 1890 walisafiri safari ngumu kuelekea Moshi (kupitia Kirua Vunjo na mto Nanga). Moshi ilikuwa ndio Makao Makuu ya ukoloni wa Kijerumani chini ya uangalizi wa Bwana Herr von Eltz. Tarehe 24 Agosti Wamisionari pamoja na Bwana Herr von Eltz waliamua kuzuru Machame. Huko Machame Wamisionari walipata fursa ya kubatiza kwa mara ya kwanza watu wachache ambao walikuwa katika hatari ya kifo (Padre Auguste alibatiza tarehe 26 na 28 Agosti). Mangi wa Machame Shangali alikula njama kisirisiri ya kutaka kuwaua Wamisionari, lakini kwa nafasi finyu Wamisionari waliweza kutoroka. Ieleweke kwamba huko Machame kulikuwa na mpasuko wa kiutawala ambapo watoto wawili (Shangali na Ngamenyi) walipigana vita kugombea nafasi ya umangi iliyoachwa na baba yao aliyefariki. 1.4.INJILI INAINGIA KIBOSHO Bwana Herr von Eltz aligundua kuwa chanzo cha ugomvi wa kiutawala huko Machame alikuwa ni Mangi Sina wa Kibosho aliyemsaidia Shangali kupata madaraka. Hivyo Bwana Herr von Eltz pamoja na Wamisionari walinuia kufika Kibosho. Sina hakuwapokea vizuri japokuwa walikaa kwa siku tatu na alitaka kuwaua, kwa bahati walitoroka na kurudi Moshi kupitia Kindi wakiufuata Mto Umbwe. Mwezi Oktoba 1892 Askofu de Courmont ambaye alikuwa akitembelea misheni ya Kilema alimpa maagizo Padre Auguste aende kufungua misheni mpya eneo la Kibosho. Ikumbukwe wakati huo vita kati ya Wachagga wa Moshi na Wajerumani ilikuwa ikifikia ukingoni (mtoto wa Mandara, Mangi Meli alijaribu kuwapindua Wajerumani). Padre Auguste hakuweza kwenda mara moja Kibosho kwa sababu alipata dharura akaenda Mombasa. Aliporudi Kilema, Padre Auguste mnamo tarehe 03 Septemba 1893 aliondoka Kilema akiwa na kundi la vijana wa kimaasai na wakichagga kuelekea Kibosho ili akausimike msalaba wa Kristo katika himaya ya Sina ambapo miaka mitatu kabla ya muda huo Padre Auguste na wamisionari wenzake Padre Le Roy na Askofu Jean Marie waliepuka makucha ya Mangi Sina ambaye alitaka kuwaua. Walipofika katika kituo cha Moshi, Bwana Herr von Eltz alipoona sehemu ya karibu ilikuwa ni Kibosho (Ngome ya Mangi Sina), alituma wajumbe wawili kwa Sinai ili kumtaarifu kwamba alikuwa anatamani azungumze naye kwa nia njema. Mwaliko huu ulimwacha Sina akibaki na mshangao asijue la kujibu, akisema “kama nikikataa pengine kutatokea vita na watu weupe (wazungu)”; “na kama nikikubali, inawezekana utawala wangu ukawa dhaifu”. Wakati huohuo, akifuatilia mambo yote kwa umakini, Sina aliwaita wazee wenye ujuzi wa kuagua na kupata ushauri kwao. Baadae akawatuma wawakilishi wake kwa Bwana Herr von Eltz akimwalika katika himaya yake. Hivyo wote kwa pamoja, wakiwa na shauku ya kumwona Sina, wakasafiri upya karibu na vyanzo vya mito mikubwa ya Kikafu, Magowa na Weruweru wakaelekea mashariki mpaka tambarare za Machame, wakaingia kwa upande wa Kindi palipokuwa na ardhi nzuri yenye rutuba (eneo ambalo halikuwa na wakazi nyakati hizo, hivyo palikuwa msitu mkubwa wa miti). Wakafika mto Umbwe ambao ulikuwa mpakani mwa himaya ya Sina. Kisha waliwaona wajumbe wa Sina wakiwasubiri hapo mpakani wakiwa na zawadi za mbuzi na mkuki. Wakiwa njiani kuelekea kwa Mangi walipishana wa watu wakifanya kazi za kilimo (hasa kilimo cha migomba), uchungaji wa wanyama na kufua vyuma. Kisha wakafika alipoishi Sina. Wamisionari hawa hawakupata mapokezi ya kifahari kama waliyopata sehemu nyingine. Baada kusubiri kwa muda mrefu ndipo Sina akatokea akitanguliwa na walinzi wake wakisindikizwa na mtoto aliyebeba kiti (LORIKA) pamoja na mkalimali. Mkalimali huyu ndiye yuleyule ambaye wamisionari hawa walikutana nae Machame (miaka mitatu iliyopita walipozuru Machame). Sina akaenda moja kwa moja kusalimiana na Bwana Herr von Eltz. Wamisionari hawa walimwelezea Sina kuwa ni jitu lenye nguvu nyingi za kimwili mwenye miaka karibia na arobaini wakati walipokutana naye. Wakaanza mazungumzo, walipomaliza walikubaliana kuwa kesho yake watafikia muafaka. Mkalimali wa wamisionari alikuwa Nderingo mtu ambaye alisafiri na hao Wamisionari akiwasaidia kubeba mizigo na pia aliwapa habari za siri kuhusu Wamangi wa sehemu tofauti tofauti. Msafara wa wamisionari ulikuwa na Waafrika arobaini baadhi yao walikuwa wabeba mizigo na wengine walikuwa askari kutoka Sudani wa Bwana Herr von Eltz. Kama ilivyokuwa desturi ya Sina kuonesha umwamba wake, aliwapitisha askari wake mbele ya Wamisionari. Wamisionari waliogopeshwa na mazoezi ya askari wa Sina hata Padre Auguste Commenginger alikaa kimya na kuingiwa na mashaka. Bwana Herr von Eltz alichoshwa sana na namna Sina alivyokuwa akiwaamuru askari wake wafanye mazoezi ya kivita, alisema “kama Sina anataka amani ni bora aseme ili tujue, na kama anataka kupigana vita atuhakikishie. Ikitokea askari wa Sina hawamalizi mazoezi, na sisi tutaanza mazoezi yetu pamoja na bunduki zetu na silaha nyingine”. Baadae kidogo Sina akatokea na walinzi wake, kisha akaamuru aongee na Bwana Herr von Eltz kwa faragha. Basi Sina alikubali kufanya urafiki na watu weupe (Wamisionari) na pia alikubali kuishi kwa amani na Wamisionari hao. Mazungumzo yakaisha, askari wa Sina wakaanza kuimba na kufanya mazoezi ya vita lakini si katika hali ya kuwakasirisha msafara wa Wamisionari. Siku hiyo wakalala kwa amani. Walipoamka asubuhi, baada ya kifungua kinywa walisindikizwa na walinzi wa Sina huku wakirudia njia ile ile ya Kindi. Baada ya kuondoka, msafara wa Wamisionari walikuwa wakikumbushana jinsi Sina alivyowachachafya. Kurudi kwao salama halikuwa jambo la kawaida kwani walipokuwa kwa Sina walijiona kama wapo mdomoni mwa simba. Hata baada ya makubaliano ya amani walidhani usiku ule askari wa Sina wangewavamia na kuwachinja wote. Mwishoni wakarudi salama kwenye kituo chao cha Moshi. Padre Auguste alifika tena Kibosho mwishoni mwa mwezi Septemba 1893. Ilimpasa awe mwangalifu sana kwa sababu miaka mitatu iliyopita Sina alishapanga kuwaua Wamisionari. Sina aliona wivu namna Wamisionari walivyoishi na Mangi Fumba huko Kilema, hivyo alituma ujumbe mara nyingi wa kuwakaribisha tena Wamisionari Kibosho. Sina mwenyewe alimteua Kipale ili asaidiane na Wamisionari. Kipale alimpa Padre Auguste makazi ya muda, Kipale alikuwa akichelewesha mchakato wa kutoa ardhi, lakini Padre Auguste aliposisitiza sana ndipo baadae akapewa sehemu ya kujenga makazi ya kudumu. Lakini katika sehemu hiyo ya kwanza aliyopewa Padre haikuwa bora kwa kituo cha uinjilishaji. Hivyo Padre Auguste akaenda kwa kiongozi wa kijerumani Moshi ili amsaidie kupata sehemu iliyo bora kuweka kituo cha uinjilishaji. Kapteni Johannes alitoa maagizo kwa Sina, ambaye alimteulia mtu aitwaye Funde (Shindi/Shundi) awasaidie Wamisionari kupata sehemu iliyo nzuri. Funde alimwonesha Padre Auguste sehemu ya sasa ambapo Parokia ya Kibosho imejengwa pamoja na taasisi nyingine za Kanisa. Padre Auguste aliishi vizuri sana na Wakibosho hata wakampachika jina jipya MAHOO (mtu mpole na mstaarabu). Mmisionari mwingine wa kukumbukwa ni Padre Martin Rohmer ambaye pamoja na Bruda Damase waliteuliwa na Askofu de Courmont tarehe 16 Januari 1894 kwenda kumsaidia Padre Auguste. Mapadre hawa wawili walifanya kazi pamoja huko Kilema, na hivyo iliwapasa pia kufanya kazi katika kituo kipya cha Kibosho. Tarehe 28 Januari 1894 Sina aliwatuma watoto watatu kwa Padre Auguste ili wapewe mafundisho ya katekesi. Padre Auguste alipoumwa na kuondoka kwa muda, alimkabidhi Padre Rohmer majukumu ya kusimamia misheni mpya ya Kibosho. Muda si mrefu Padre Rohmer hakuelewana na Sina. Sababu ya kutoelewana ilikuwa ni mfereji ulioleta maji kwenye kituo cha misheni. Watu walizuia maji yasifikie kituo cha misheni. Hivyo, Padre Rohmer aliomba msaada kwa Sina, lakini Sina alionyesha hali ya kutojali tatizo la Padre Rohmer.Pia kuna kipindi Sina aliwahamasisha watu wake wasiwauzie vyakula Wamisionari. Padre Auguste alirudi Kibosho tarehe 8 Februari 1894, kisha alifahamu kuwa Sina hahusiani vizuri na Padre Rhomer. Moyoni mwake Padre Auguste alitambua ugumu na kazi nzito katika misheni ya Kibosho ambayo ilimhitaji mtu mwenye kuvumilia magumu kama Padre Rohmer. Kwa jinsi alivyovumilia magumu na kupambana na Sina, wenyeji wa Kibosho walimwita NKINGIRI (nguruwe mwitu), kwa sababu Padre Rhomer alikuwa na kichwa kikubwa na ndevu ndefu zenye rangi inayokaribiana na nyekundu. ENEO Parokia ya Kibosho kwa upande wa kaskazini imepakana na Seminari kuu ya Falsafa ya Bikira Maria Malkia wa Malaika Kibosho kusini ni kapelano ya Mt. Patrice singachini, masharika bonde la hifadhi la mto Nsoo, Parokia teule ya Mt. Agness Mweka. Magharibi ni bonde la hifadhi la mto Karanga, Parokia ya Mt. Anna Kirima, Parokia ya Roho Mt. Mango na Parokia ya Franciss Xsavery-Nkombole zinazopakana na Kigango cha Mt. Martine wa Pores - Otaruni.

JH1C9376.JPG
JH1C9376.JPG

Shughuli za kichungaji

Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Kibosho ni moja ya Parokia kongwe katika Jimbo Katoliki Moshi na inayotegemewa kuwa Parokia iliyokomaa kiimani. Kufikia lengo la kuwa Parokia imara basi mpango mkakati ulioandaliwa umegawanywa katika sehemu kuu nne (4):

  1. Kuhimiza maisha ya sala na kazi.

  1. Tafakari ya Neno la Mungu.

  1. Mkazo katika malezi mfungamano (integral formation) kwa makundi yote ya waamini.

  1. Kuwajengea watu dhamiri njema haki/umoja/amani (Rejea Sinodi ya Maaskofu).

Ratiba ya Misa

MISA

                Jumapili

  • Misa ya I     saa.    11:30 alfajiri

  • Misa ya II    saa.    01:00 asubuhi

  • Misa ya III   saa.    03:30 asubuhi

  • Misa ya IV  saa.    04:30 asubuhi

  • Jumatatu hadi Ijumaa Mapadre wanapatikana muda wote kwa mpangilio.

  • Huduma nyingine za kiofisi zinatolewa na Sista na Katekista kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa saa 1:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana.

  • Jumamosi ni siku ya huduma kwa wanafunzi wa Komunyo /Kipaimara, Mt Alois, Bikira Maria na Utoto wa Yesu.

  • Jumatano ya mwisho ya kila mwezi katika muda wa saa 1: 00 hadi saa 2:00 usiku ni siku ya ibada ya sakramenti ya kitubio na upatanisho  kwa wanafunzi na wanachuo wote Kanisani.

  1. Kuabudu na baraka ya sakramenti kuu pamoja na kusali masifu ya jioni (vespers) ni kila Dominica saa 10:00 jioni hadi saa 11:00 jioni.

  2. Ijumaa ya kwanza ya mwezi ni kuabudu kutwa nzima baada ya misa ya kwanza na kuhitimisha saa 10:00 jioni kwa masifu ya jioni na baraka.

Ratiba ya kukutana kwa adhimisho la misa takatifu kwa kila mtaa kwa kila mwezi ni kama ifuatavyo:-

  1. Kanda ya SINGA JUU             Jumatatu  ya pili ya kila mwezi

  2. Kanda ya HOSPITAL              Jumatano  ya mwisho ya kila mwezi

  3. Kanda ya  SINGA KIFUENI   Jumamosi  ya mwisho ya kila mwezi

  4. Kanda ya SINGA KATI           Jumattatu  ya mwisho ya kila mwezi

  5. Kanda ya MAUA                     Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi

PICHA ZA KANISA NA MAZINGIRA

IMG_2521_edited.jpg

Ndiyo, ikiwa watu wawili au watatu wanaoniamini watakusanyika pamoja, mimi nitakuwa pamoja nao

Mathayo 18:20

Wasiliana nasi

St Marys Kibosho Parish, Kibosho

Tumsifu Yesu Kristu!

bottom of page